Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Thursday, May 31, 2012

Maaskofu watema cheche Zanzibar


Maaskofu
Maaskofu wa madhehebu ya Kikristo Tanzania wametoa tamko la kuitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwasaka watu wanaofanya vitendo vya kuhujumu makanisa na kutishia usalama wa waumini na umoja wa kitaifa.

Tamko hilo limetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, kwa niaba ya viongozi wenzake wa madhehebu ya Kikristo mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, ofisini kwake jana.

Askofu Mokiwa alisema tangu kuanza kulipuliwa kwa makanisa, waumini wa Kikristo wamekuwa wakiishi Zanzibar kwa hofu na kwamba hakuna hatua zilizochukuliwa za kuwakamata na kuwafikisha mahakamani waliohusika na vitendo vya uchomaji moto makanisa na urushaji wa mawe.

Alisema vitendo hivyo vimekuwa vya kawaida na kuwafanya waumini wa Kikiristo Zanzibar kuishi kwa hofu na kuonekana kama raia wa daraja la pili mbele ya haki ya kikatiba, huku serikali ikishindwa kuchukua hatua tangu mwaka 2001.

"Vitendo vinavyoendelea hatujui, tufahamu vipi ama serikali inavipenda, inavifurahia au ina mkono wake katika matukio haya:” alisema na kuongeza: “Sijui mnatutaka tuwe na mtazamo gani kuhusu Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar, zaidi ya makanisa 25 yamehujumiwa kwa kuchomwa moto, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa licha ya kuripoti katika vituo vya Polisi.”

Alisema matukio hayo hivi sasa yanajenga hisia kuwa Mkristo Zanzibar ni sawa na kuishi ukiwa na hofu. “Hatuthamini hata wawekezaji kutoka Tanzania Bara wanapotaka kuwekeza ama kufungua maduka ya kuuza vinyago, wanapobainika Wakristo hunyimwa vibali na matukio ya kurushiwa mawe wakiwa kanisani,” alisema.

Tamko hilo lilisema kuwa watu wanaofanya vitendo vya hujuma siyo wahuni, siyo wendawazimu, bali ni watu ambao wana ajenda maalum na serikali lazima iwasake ili kujenga imani kwa wananchi wasiopenda vurugu na machafuko.

"Mambo ya kukashifiana sasa basi, tumechoka, tumechoka, tena tunasema tumechoka kwa herufi kubwa, serikali lazima idhibiti mihadhara yenye uchochezi na kuwagawa watu, tunawaomba Masheikh walikemee jambo hili kwa waumini wao,” alisema Dk. Mokiwa.

Alisema kampeni inayofanywa ya kutaka watu kutoka Tanzania Bara waondoke Zanzibar ni jambo la hatari kubwa ambalo litavuruga umoja wa kitaifa.

“Ni kauli hatari sana, kusema watu kutoka Tanzania Bara waondoke Zanzibar wakati kuna Wazanzibari na Wapemba wanajenga nyumba na kuendesha biashara Tanzania Bara, tena wengine hata Zanzibar hawajajenga wala hawajawekeza kama walivyojenga Tanzania Bara,” alisema askofu huyo.

Alisema ukiona bubu anasema kwa vidole ujue amechoka na sasa siyo wakati tena wa serikali kucheka na watu wanaohatarisha umoja wa kitaifa, bali wakamatwe, wapigwe bakora na polisi na baadaye wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Askofu Mokiwa alisema yako mataifa yameingia kwenye vurugu kubwa kutokana na chockochoko za imani za dini, na kuelezea kuwa kama tatizo ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ni vyema zikatumika njia bora ambazo tayari serikali imeziweka ikiwemo kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akifanya majumuisho, Waziri Aboud aliwashukuru viongozi hao kwa kuonyesha uvumilivu na kuwataka wawe na subira katika kipindi hiki ambacho serikali ikiendelea kudhibiti vitendo hivyo ikiwemo kuweka ulinzi katika nyumba za ibada.

Alisema tamko hilo atahakikisha analifikisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein, kama walivyotaka maaskofu hao na kusisitiza kuwa serikali haitakubali kuwavumilia wale wote wenye lengo la kuhatarisha amani ya nchi pamoja na kuwatia wasiwasi waumini wa dini nyingine.

Alisema vitendo hivyo havivumiliki na vinakwenda kinyume cha katiba kwa sababu serikali haina dini bali wananchi wake ndio wenye dini na wana uhuru wa kuabudu kulingana na imani zao.

Alitoa mfano kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo kujengwa kanisa katika eneo la Mbweni mwaka 1870 na kwamba walioruhusu ujenzi wa makanisa ni wafalme ambao walikuwa ni Waislamu.

Alisema Zanzibar ina historia nzuri kati ya Waislamu na Wakristo, ikiwemo kushirikiana wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambako hakuna Mkristo anayekula mchana na wakati wa sikukuu Wakristo husherehekea sikukuu za Waislamu sambamba na Waislamu kusherehekea sikukuu za Wakristo kama vile Krismas na Pasaka.

Kuhusu Rais wa Zanzibar, Waziri Aboud alisema amekuwa akichukua hatua za kukemea vitendo vilivyokuwa vikifanywa na Jumuiya ya Uamsho katika mikutano mbalimbali ya hadhara kisiwani unguja na Pemba, lakini viongozi hao wameshindwa kuheshimu sheria na katiba za nchi.

Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetaka viongozi wa vyama vya siasa na taasisi za dini na jumuiya za kiraia Zanzibar kudumisha ushirikiano kulinda amani na umoja wa kitaifa wa Watanzania.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Hamad Mussa Yusuph, alisema vurugu zilizotokea Zanzibar zimefanywa kwa makusudi na vijana ambao wanaonekana walishapata mafunzo katika kipindi cha nyuma.

Alisema vyama vya siasa viache kuunda makundi ya vijana ambao mwisho wake wanakosa kuwapatia kazi na mwisho wake kuanza kufanya vitendo vya uhalifu zikiwemo fujo kama zilizotokea.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Kampuni ya Fresh Enterprises, Catherina Peter, alisema wamiliki wa baa wanaishi kwa wasiwasi kutokana na vitendo vya hujuma ambavyo vimekuwa vikifanyika katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari, alisema baa ya Daraja Bovu ilivamiwa na kuibiwa milango, madirisha na masinki ya vyoo na kuitaka serikali ifanye uchunguzi wa kina kuwabaini watu waliofanya hujuma hizo Zanzibar.

Baadhi ya maaskofu waliokuwepo katika mkutano huo ni Askofu Augustino Shao wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Askofu Dickson Kaganga wa Tanzania Assemblies of God na Askofu Michael Hafidhi wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Zanzibar.

DCI MANUMBA ATOA ANGALIZO

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, amesema iwapo viongozi wa kisiasa, kidini na wanajamii hawatashiriki kikamilifu kuilinda na kuitetea amani ya nchi, ipo siku vizazi vijavyo vitalia, kutukana na kuyachapa makaburi yao viboko.

Manumba alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa dawati la jinsia na watoto katika kituo kikuu cha polisi Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro kilichojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNCEF) na Jeshi la Polisi nchini.

Alisema takwimu za kila siku kitaifa zinaonyesha kuna idadi kubwa ya matukio yanayoashiria uvunjaji wa amani ya nchini, ambapo baadhi ya viongozi wa kisiasa, kidini wanashabikia kwa madai ya kutetea itikadi zao huku kukiwa na ongezeko la maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu kudai mikopo pamoja na maandamano katika shule za msingi na sekondari.

“Utangamano wa kitaifa, amani na utulivu ni jukumu letu sote, tukiichezea amani iliyopo kwa malengo yetu binafsi au kikundi fulani, vizazi vijavyo vitalia juu ya makaburi yetu huku vikiyachapa viboko, tuangalie tumetoka na tunakwenda wapi kwa faida ya nchi, kila unapokaa na mwenzako zungumza naye aache kufanya mambo yenye kuhatarisha amani,” alisema Manumba.

Alisema yapo matukio mengi ya wananchi wanaojiita wenye hasira kali ambao kuchoma moto wezi, mauaji ya albino na vikongwe kwa imani za kishirikina pamoja na wanaovamia vituo vya polisi na kwa lengo la kutaka kuwatoa waalifu ili wawaue na mwishowe kuchoma vituo vya polisi.

0 comments:

Post a Comment