Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Friday, October 7, 2011

Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI)

Imeelemewa na wagonjwa kutokana na kuongezeka kwa kasi za ajali za barabarani na kusababisha wengi wa wagonjwa hao kulazwa chini kwa kukosa vitanda. Hali hiyo ilishuhudiwa na NIPASHE jana ambapo wodi zote tatu zinazotumika kuwahudumia wagonjwa wa kawaida zimeonekana zikiwa zimejaa wagonjwa na wengine kulazwa chini. Wodi ambazo zimeonekana kuelemewa na wagonjwa ni pamoja na namba 2 Jengo la Kibasila, Wodi 17 na 18 Jengo la Sewahaji. Akizungumzia hali hiyo, Afisa Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa, alisema msongamano wa wagonjwa kwenye Taasisi hiyo umekuwa katika kiwango cha juu kuliko wakati wowote na kusababisha utaratibu wa utoaji huduma kubadilishwa. Alisema kwenye wodi za Taasisi hiyo kuna vitanda vya kulaza wagonjwa wasiopungua 30 kwa wakati mmoja kila moja, lakini sasa wanalazwa zaidi ya wagonjwa 50. Alisema ongezeko la ajali limekuwa la kasi ambapo kwa kila siku wanapata wagonjwa zaidi ya 10 kwa siku wanaotokana na matukio ya ajali za pikipiki na magari. “Ni mwaka tunaoshuhudia kiwango cha ajali kipo juu na kusababisha Taasisi yetu kupokea majeruhi wengi kuliko mwaka wowote na kutufanya tuanze kupanga mikakati ya kumudu kuwahudumia,” alisema. Jumaa alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa MOI umeamua kufanya marekebisho ya kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma ya upasuaji wa saa 24 toka mgonjwa afikishwe hapo. Alisema upasuaji huo umewezesha wagonjwa kuruhusiwa mapema na kuacha nafasi kwa wagonjwa wengine wanaohitaji huduma hiyo. "Hapo zamani tulikuwa tuna utaratibu wa kumnyoosha kwanza mgonjwa kabla ya kumfanyia upasuaji, lakini kutokana na wimbi hili, utaratibu huo umebadilishwa sasa ndani ya siku moja mgonjwa anafanyiwa upasuaji na kuungwa kiungo kilichovunjika," alisema. Alisema katika mkakati mwingine, wameamua siku ya mapumziko ya Jumamosi na Jumapili, madkatari wanatakiwa kuingia kazini kama kawaida na kuunda kambi maalum za upasuaji ili kuokoa maisha ya wagonjwa. Alisema kuanzishwa kwa huduma hizo kumepunguza kwa kiasi fulani msongamano wa wagonjwa, lakini kutokana na kuendelea na kasi ya ajali bado wodi zinaendelea kujaa. "Madaktari kwa sasa hawana muda wa kupumzika kwani kambi hizi zimesaidia sana kupunguza watu wanaohitaji upasuaji na bado tunaendelea kufanya kwa siku zote za mapumziko," aliongeza. Pamoja na hayo, Jumaa alieleza mkakati wa mwingine wa muda mrefu ambao wamejiwekea kuwa ni kuongeza idadi ya wodi kwa kujenga majengo mapya. Afisa huyo Uhusiano alivitaka vyombo mbalimbali vya usalama barabarani kufanya jitihada kubwa za kudhibiti vitendo vinavyosababisha ajali. Alisema kama vyombo hivyo vitachukua hatua kwa haraka na kuwachukulia sheria madereva wasioafuata sheria za barabarani, ni wazi ajali hizo zitapungua na kusababisha hata utoaji huduma kwenye Taasisi hiyo urejee kama kawaida yake

0 comments:

Post a Comment