Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Saturday, October 8, 2011

Polisi waua raia, askari watatu nao wajeruhiwa

Mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika mapambano kati ya wananchi waliofukuzwa kwenye machimbo ya dhahabu ya Nyaruyeye, Wilaya ya Geita, mkoani Mwanza na polisi. Mtu huyo mkazi wa Kijiji cha Nyarugusu, wilayani humu, amefahamika kwa jina moja la Yahya. Katika mapambano hayo, pia askari polisi watatu, akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nyarugusu, Inspekta Msaidizi Ibrahim Mbulu, walijeruhiwa kwa mawe yaliyokuwa yakirushwa na wanachi hao. Mapambano hayo yalianza saa 3:00 asubuhi jana baada ya wananchi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 400 wakiwa na silaha mbalimbali, zikiwamo fimbo na mawe, kuvamia kituo cha Polisi cha Nyarugusu, kwa lengo la kukichoma moto na kuwashambulia askari. Hata hivyo, kabla ya kufika kituoni mita kama 400, walimwagia mafuta ya petroli juu ya bati ya nyumba za baadhi ya wananchi, ikiwamo nyumba mpya ya kulala wageni inayomilikiwa na Evarin Evarist. Nyumba nyingine inamilikiwa na Baraka Nyandu. Hata hivyo, kabla ya kuwasha moto, polisi walifika na kufanikiwa kuwadhibiti, kitendo kilichoongeza hasira kwa wananchi hao na ndipo walipoanza kwenda kwenye kituo cha polisi. Hali hiyo iliwafanya polisi kuanza kujihami kwa kupiga risasi za moto hewani baada ya wananchi hao kuanza kurusha mawe. Katika tukio hilo, gari la polisi aina ya Land Cruiser 110 lililotokea mjini Mwanza likiwa limebeba askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), lilivunjwa vioo vya mbele na ubavuni kwa mawe. Magari mengine mawili ya raia, aina ya Canter na Toyota Pick Up, yalivunjwa vioo kwa mawe. Wananchi hao walitoka katika Kijiji cha Nyaruyeye na kwenda kwenye mgodi huo uliofungwa na kutaka kuingia kwa nguvu. Hata hivyo, askari polisi wanaolinda mgodi huo walianza kurusha risasi hewani kuwatawanya. Baada ya kutawanywa, wananchi hao walijikusanya upya na kwenda kushusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya tawi la Nyaruyeye na kuichoma moto kisha wakachukua bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuipeperusha wakidai kwamba wamechoshwa na sera za CCM. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alithibitisha matukio hayo na kuwa askari walikuwa wamepelekwa kuongeza nguvu. Alisema ulinzi ni wa halali kwa vile eneo hilo liko kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, Kamanda Barlow aliahidi kuwa atatoa taarifa zaidi za tukio hilo baadaye

0 comments:

Post a Comment