Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Friday, October 7, 2011

MATOKEA YA IGUNGA

MATOKEO ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Igunga, mkoani Tabora yalitangazwa jana ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliibuka mshindi kikifuatiwa kwa karibu na Chadema, huku vyama vingine vilivyoshiriki katika kinyang’anyiro hicho vikitupwa mbali. Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliochukua mwezi mmoja, Msimamizi wa uchaguzi huo, Protase Magayane alisema CCM kilipata kura 26,484 na Chadema kura 23,260 wakati Chama cha Wananchi (CUF) kilipata kura 2,104. Vyama vingine vitano vilivyoshiriki vilishindwa vibaya kwa kugawana jumla ya kura 739 tu, kwani kura 1,185 ziliharibika. Tunavipongeza kwa dhati vyama vyote vilivyoshiriki katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa kuliko chaguzi nyingine zozote katika historia ya jimbo hilo. Ushindani huo ulikuwa mkubwa mno kiasi cha kuleta hofu miongoni mwa wananchi kutokana na vitendo vilivyoashiria kuwapo kwa uvunjifu wa amani. Kutokana na kuwapo kwa purukushani wakati wote wa kampeni, macho na masikio ya Watanzania yalielekezwa Jimbo la Igunga. Vyombo vya habari vililitangaza sana Jimbo la Igunga na kulifanya liwe moja ya sehemu maarufu sana hapa nchini kutokana na uchaguzi huo. Hofu hiyo ilisababishwa na vyama vya CCM, Chadema na CUF ambavyo, pengine katika kutafuta ushindi kwa kutumia mbinu za msituni, vilichezeana rafu na kufanyiana visa kiasi cha kuzitia majaribuni mamlaka zote zilizokuwa zinasimamia uchaguzi huo. Lakini katika hali ya kushangaza, mamlaka hizo kwa mara ya kwanza zilisimama katikati na kutoa haki kwa vyama vyote bila kuegemea upande wowote.Viongozi wake walituliza vichwa na ndiyo maana hatukuona wanababaishwa au kuyumbishwa na propaganda chafu zilizokuwa zinapikwa na vyama hivyo. Tulishuhudia, kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi katika nchi yetu mwaka 1992 Jeshi la Polisi likifanya kila lililoweza kuchukua hatua stahiki bila kukurupuka, kukipendelea chama tawala au kuvikandamiza vyama vya upinzani. Hata kama ulijitokeza udhaifu wa hapa na pale lazima tukiri kwamba, udhaifu huo ulitokana na ubinadamu na siyo vinginevyo. Kazi hiyo ya kujivunia ya jeshi hilo pia iliboreshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ambayo ilitangaza mapema kwamba chombo hicho kingesimamia haki kwa kuhakikisha kinatangaza matokeo haraka iwezekanavyo na kwamba kingemtangaza mshindi wa kweli pasipo kupindisha matokeo. Ndiyo maana uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu licha ya kutawaliwa na minyukano mikali wakati wa kampeni. Na bila shaka ndiyo maana viongozi wa vyama hivyo vilivyoshiriki katika uchaguzi huo vimekubali matokeo, kinyume na ilivyokuwa huko nyuma wakati matokeo ya chaguzi mbalimbali yalionekana dhahiri kwamba yamepikwa ili kuwabeba wagombea wa chama tawala. Sisi tunadhani huu hasa ndiyo ushahidi wa kukua kwa demokrasia katika nchi yetu na ni ishara tosha kwamba, iwapo itapatikana Katiba mpya, amani na utulivu vitashamiri milele kwa vizazi vilivyopo sasa na vitakavyokuja baadaye. Tunazishauri mamlaka zenye dhima ya kusimamia chaguzi mbalimbali kuhakikisha mapungufu yote yaliyojitokeza jimboni Igunga yanaondolewa kabla ya kufanya chaguzi nyingine. Kwa mfano, lazima Daftari la Wapigakura lipitiwe upya kabla ya chaguzi kufanyika ili ziwepo takwimu sahihi za wapigakura wapya, waliohama, waliohamia, waliofariki au waliopoteza kadi za kupiga kura. Hivi sasa kuna mashaka iwapo idadi ya wapigakura waliomo katika daftari hilo ni sahihi au ni ya kupikwa kwa sababu za kisiasa. Daftari lililotumika katika uchaguzi wa Igunga linatia mashaka na Mungu bariki udhaifu huo haukutumiwa na wapinzani kuyakataa matokeo. Maswali mengi bado yanaulizwa kuhusu sababu zinazowafanya watu wengi waliojiandikisha kupiga kura kutofanya hivyo katika chaguzi mbalimbali zilizopita. Katika uchaguzi wa Igunga, kwa mfano, waliojiandikisha ni 171,019 lakini waliopiga kura ni 53,672 ambayo ni asilimia 31.3 tu ya watu waliojiandikisha. Kasoro hii ni kubwa. Ni matumaini yetu kwamba Serikali itaipa changamoto hii kipaumbele stahiki kwani ni kiashiria tosha cha vurugu na umwagaji damu katika siku za usoni.

0 comments:

Post a Comment