Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Wednesday, September 21, 2011

Zitto aibana serikali ifafanue kauli ya kupanda kwa umeme


Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na Waziri wa Nishati na Madini, Willim Ngeleja, kutoa ufafanuzi kwa umma juu ya tamko la kupanda kwa bei ya umeme lilitolewa juzi na Waziri Mkuu. Zito alisema hayo, kufuatia kauli ya Waziri Mkuu aliyoitoa juzi wakati akiwahutubia wakazi wa Musoma kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Mukendo. Katika Mkutano huo Pinda alisema bei ya umeme itapanda wakati wowote kutokana na Serikali na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kubeba mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji. Zito alisema, lazima serikali ifafanue vizuri kuhusiana na kupanda kwa bei hiyo ili isiwaumize wananchi wa kawaida ambao matumizi yao ni madogo ukilinganisha na wafanyabiashara wakubwa hususani makampuni na wale wenye biashara kubwa. “Tunamuomba Waziri Mkuu Pamoja na Ngereja waufafanulie umma, kuhusiana na ongezeko la bei ya umeme kwa sababu endapo watasema ongezeko hili litapanda kwa wananchi wote watakuwa wamewaumiza wale wenye kipato cha chini,” alisema Zitto jana katika mkutano wa kujadili nishati ya umeme, madini na miundombinu Alisema katika kila saa 24 hivi sasa taifa hupoteza Dola milioni 400 kutokana na tatizo la mgawo wa umeme, ambapo katika kila megawati 1 ni sawa sawa na Dola 2 za Kimarekani.
CLEOPA MSUYA: NI AIBU NCHI KUKAA GIZANI
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya, alisema ni jambo la aibu kuona kwamba taifa linaendelea kukaa gizani. “Ni jambo la kushangaza kuona kwamba taifa linaendea kukaa katika giza wakati nchi imesheheni vyanzo na mali asili nyingi, mpaka sasa ni asilimia 14 tu ya watanzania ndio wanapata umeme, lakini asilima 86 hawana umeme, kwa kweli hili lazima liangaliwe upya,” alisema na kuongeza: “Sasa hivi tunasheherkea miaka 50 ya uhuru, taifa bado linakabiliwa na changamoto nyingi. Ajira kwa vijana bado ni tatizo kubwa, vijana wengi hawana ajira, tatizo la umeme nalo ni shida kubwa. ukiangalia katika ukuaji wa uchumi nalo ni shida, na bado tunaendelea kuimba kukuza uchumi, lazima utafutwe mwafaka wa mambo haya bila hivyo taifa litaingia katika matatizo makubwa.” Aidha Msuya aliongeza kuwa ili changamoto zinazoikabili taifa hivi sasa zitatuliwe, ni lazima kuongeza ajira kwa vijana ambao kwa namna moja ama nyingine wataingia katika ushindani kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika masuala ya kukuza uchumi hususani sekta za nishati, madini na miundombinu.
SUMAYE: TUFANYE KAZI KWA BIDII
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alisema watanzania hawana budi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kwamba wanaleta mabadiliko. “Hatutaweza kushindana katika soko la pamoja endapo hatutajidhatiti kufanya kazi kwa bidii, kutengeneza bidhaa bora, lazima twende katika biashara kwa nguvu zote, bila uvivu na tuweke mfumo ambao utatupeleka pazuri, tusilale,”alisema na kuongeza: “Pia tunaomba sekta binafsi iungane na serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili nchi sasa hasa katika masuala ya nishati ya umeme, sekta binafsi ni kama injini hivyo endapo itashiriki ipasavyo, tatizo la umeme litakwisha.”

0 comments:

Post a Comment