Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Wednesday, September 21, 2011

Wachezaji Yanga watapika nyongo

  Tegete arejeshwa kundini

Baada ya makocha wa Yanga, Sam Timbe na msaidizi wake Fred Minziro, kuwekwa kitimoto na uongozi wa klabu hiyo juzi kuhusiana na matokeo mabovu waliyopata katika mechi walizocheza za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, jana kibao kiliwageukia wachezaji wa timu hiyo ambao nao walilazimika kutoa maelezo mbele ya viongozi wa klabu hiyo. Habari zilizopatikana jana jioni zinaeleza kuwa makocha hao waliueleza uongozi kwamba wanashindwa kuelewa ni kwa nini washambuliaji wao wanashindwa kufunga mara kadhaa wanapofika karibu na lango la wapinzani na kufanya mwisho wa mchezo watoke uwanjani na matokeo yasiyoridhisha. Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa Timbe na wenzake wa benchi la ufundi, waliweka wazi kwamba wachezaji wao wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri mazoezini na pia katika mechi hutengeneza nafasi za kufunga, lakini umaliziaji umekuwa tatizo kwao. 
Jana jioni, wachezaji wa timu hiyo ambao hufanya mazoezi asubuhi, waliitwa na kamati ya utendaji ya klabu hiyo pamoja na kamati ya ufundi ili kueleza kinachowasibu na kujikuta katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi. Wachezaji hao, kwa nyakati tofauti walikuwa wakisimama na kutapika nyongo zao, wakieleza kile wanachoamini kuwa ndicho kinachowapa matokeo mabaya. Kinyume na hofu za baadhi ya ‘wanajangwani’ kuwa pengine kuna kitu kinawakera, inaelezwa kwamba wachezaji walisema wazi kwamba wao hawana malalamiko yoyote dhidi ya uongozi. Badala yake, chanzo kinadai kuwa wachezaji walisema kinachowaponza ni ‘upepo mbaya’ tu kwani kama kujituma uwanjani, wao hujituma sana katika kila mechi ili waibuke na ushindi. Nyota mwingine alipendekeza kuwa wanachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kumuomba Mungu ili jitihada zao ziwape ushindi katika mechi zinazofuata na kurejesha utulivu, huku akikiri kwamba ushindani uliopo dhidi ya timu wanazokutana nazo ni mkubwa kuliko watu wengi wanavyodhania. Nyota hao ambao Julai walitwaa taji la klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), walikumbushia vilevile kuwa ushirikiano wa pande zote, kuanzia kwa viongozi, wanachama, wachezaji na wapenzi, ni jambo muhimu kwa sababu kila mmoja ana mchango wa kuifikisha Yanga kwenye mafanikio. Wakati huo huo, uongozi wa klabu hiyo, ulimrejesha kundini mshambuliaji Jerryson Tegete juzi, na jana asubuhi alianza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao ya ligi kuu watakayocheza leo dhidi ya Villa Squad kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam. Septemba 12 mwaka huu, uongozi wa klabu ya Yanga ulitangaza kumsimamisha Tegete kwa mwezi mmoja kwa kosa la utovu wa nidhamu. Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwa wamefikia uamuzi wa kumrejesha Tegete baada ya kuandika barua ya kuomba radhi ambayo ilifikishwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya Yanga iliyokutana juzi jioni na makocha wa timu hiyo. Tegete aliliambia gazeti hili kwa kifupi kwamba amerejea kikosini na ataendelea kujituma ili timu yake ipate matokeo mazuri katika mechi zinazoendelea. "Ni kweli nimerejea na nimefanya mazoezi leo (jana) asubuhi na wenzangu… mambo yaliyotokea yamemalizika," alisema kwa kifupi mshambuliaji huyo aliyejiunga na Yanga akitokea katika Shule ya Sekondari ya Makongo iliyopo jijini Dar es Salaam. Habari zaidi ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa Yanga kuhusiana na mwenendo mbovu wa timu yao, zinasema kwamba ligi ya msimu huu ni mgumu na kwamba hakuna mgomo wowote unaofanywa na wachezaji kama inavyodaiwa na baadhi ya watu. Yanga ambayo imeshinda mechi moja dhidi ya African Lyon, ina pointi sita tu baada ya kucheza mechi sita na hivyo inakamata nafasi ya 11 kati ya timu 14 kwenye msimamo wa ligi.
Wakati Yanga wakisuasua kwa kushika nafasi ya karibu zaidi na ukanda wa kuteremka daraja, watani zao wa jadi, Simba wako kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi sita kama Yanga, wakifuatiwa na Mtibwa na Azam waliofikisha pointi 11 baada ya kila mmoja kucheza mechi sita pia.

0 comments:

Post a Comment