Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Tuesday, September 20, 2011

Sababu za wanafunzi kufeli hesabu hizi hapa


 

Mtaalamu wa hesabu za Aljebra na mwanaharakati wa elimu, Nderakindo Kessy
UFAULU mdogo wa somo la Hisabati kwa wanafunzi katika madaraja ya elimu ya msingi na sekondari unatajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya elimu nchini.
Licha ya kuwapo juhudi mbalimbali za Serikali kukuza somo hilo,tafiti na uzoefu vinaonyesha wanafunzi wengi katika madaraja hayo wanaendelea kufanya vibaya katika somo hilo.

Mtaalamu wa hesabu za Aljebra na mwanaharakati wa elimu, Nderakindo Kessy anatoboa siri ya maendeleo duni ya somo hilo kama alivyohojiwa na mwandishi wetu Fredy Azzah.

Swali: Kwa  uzoefu wako ukiwa mtaalamu wa hesabu, nini chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya katika somo la Hisabati?
Jibu: Sababu ni nyingi, lakini kubwa zilizopo ni kutokuwepo kwa mtalaa na uandishi mbovu wa vitabu.  Kuna kampuni moja iliwahi kunipa kazi ya kuhariri vitabu vya Hisabati vya shule ya msingi ambavyo vilikuwa ni vya darasa la nne mpaka la saba.

Hapo ndipo nilipojua kwamba, tatizo moja kuu la watoto wetu kutojua Hisabati, linatokana na ubovu wa vitabu. Mfumo mzima wa utayarishaji wa vitabu vya Hisabati, unadumaza uwezo wa wanafunzi katika kukuza vipaji vyao kwenye somo hilo.

Kwa mfano,  nilichokigundua karibu vitabu vyote  kuanzia darasa la tatu hadi la saba, vinaandika kwamba tafsiri ya Ten thousand (elfu kumi), ni makumi elfu, badala ya maelfu kumi. Hii inavuruga mtiririko wa dhana ya viwango vya thamani vya namba nzima.

Lakini pia, kuna tatizo kati ya tarakimu na namba, waandishi wanaandika 273, wanasema chukua namba ya kwanza, badala ya kusema chukua tarakimu ya kwanza.
Tatizo hapo linakuja kwenye kujenga concept (wazo), mtoto anakuwa anachukua mambo kwa jumla jumla tu, anakosa uwezo wa kuchambua jambo kwa undani wake.

Mtoto akikwambia, kuna mtu amekuja hapa kukuulizia na mwingine akasema kuna mtu  mwanamke aliyekuja kukuulizia, unajua kabisa huyu wa pili ana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo.
Unaambiwa karibu asilimia 25 ya watoto wanaomaliza darasa la saba, hawajui kufanya hesabu za kujumlisha namba mbili nzima.

Janga hili ni kubwa kuliko tatizo la umeme ambalo lipo nchini sasa hivi. Kama mwanafunzi anaweza kujumlisha 5 na 7, kwa nini ashindwe 50 na 70?

Swali: Umetaja mtalaa kama sababu inayozorotesha somo hili, wafafanulie wasomaji?
Jibu:
Katika harakati zangu, nimebaini kwamba sisi hatuna mtalaa, tuna kabrasha linaloitwa muhtasari wa mtalaa, lakini mtalaa wenyewe hakuna. Sijui huu ni muhtasari wa kitu gani, kwa sababu inatakiwa muhtasari uwe wa kitu fulani.
Na hii ndiyo moja ya sababu kuu ya vurugu hizi za utayarishaji wa vitabu. Mtalaa ndio unaotakiwa uelekeze kuwa jambo fulani lifanywe vipi, mtaala unatakiwa utoe maelezo ya kina na muhtasari uyaeleze kwa ufupi.
Mwalimu akiulizwa jambo fulani na  akawa hana  majibu ya kutosha, aende kwenye muhtasari ambao na wenyewe utamrejesha kwenye mtalaa ili apate maelezo ya kina.

Kubadilika kwa silabasi siyo tatizo, kwa sababu huu ni mtiririko tu. Kama kungekuwa na mtalaa, hiyo silabasi ingeufuata huo mtalaa jinsi unavyotaka.
Mtaala ni sawa na Katiba, sheria zitungwe kadri watu wawezavyo,  lakini zisiathiri sheria mama ambayo ni Katiba, mwongozo wote utakuwa unatoka kwenye mtalaa.

Kinachonisikitisha ni kuona hata viongozi wakubwa tu wakiimba wimbo wa mitalaa mibovu,  wakati hatuna hicho kitu, wanawaimbisha wananchi  wimbo usiokuwa na maana.
Naomba hao wabunge na wengine wanaosema mambo ya mitalaa mibovu, waombe kupewa hiyo mitalaa kama wataiona.
Swali: Tatizo kubwa linaonekana lipo upande wa mtalaa, kipi kikubwa kilichopo katika mtalaa?
Jibu: Nimeshasema, mtalaa ni sawa na Katiba, unatakiwa umwambie mwalimu  mbinu za kufundisha ni hizi na hata vifaa gani atumie.Kwenye shule zetu,  watoto wa darasa la kwanza unakuta wanaenda shule wakiwa wamebeba mzigo wa visoda ama vijiti.

Mwalimu  anamwambia mwanafunzi ahesabu vidole, kwamba vidole vitano ukiongeza vitano unapata 10. Ni kosa kubwa sana kumfundisha mtoto kwa kuhesabu vidole, vijiti au visoda.
Kila namba mwanzo wake ni sifuri, sasa unapomwambia mtoto ahesabu vidole, inatakiwa kwanza umwambie kidole sifuri ni kipi, pia cha kwanza na cha mwisho ni kipi.

Kuna njia nyingi unazoweza kuzitumia  kumfundisha mtoto hesabu bila hivyo vidole wala vijiti na mtoto akaelewa kabisa kila unachotaka ajue.

Walimu wakipatiwa mafunzo inawezekana. Kwa hili la hesabu kwa mfano,  kinachohitajika ni kipande kidogo cha karatasi ambacho mwalimu ataandika  namba sifuri mpaka 20 kwa mtiririko maalum,  kisha atumie kumfundishia mtoto.

Kuhesabu vijiti na vidole ni ufundishaji potofu, kama kungekuwa na mtalaa unaowaelekeza walimu jinsi ya kutumia mbinu nyingine ambazo zipo, watoto wetu wangekuwa mbali sana.
Huu muhutasari tulio nao unasema chukua vitu 100,000 ongeza 700,000,  sasa sijui mtoto aliyefundishwa kwa kuhesabu vidole atawezaje kufanya hiyo kazi.

Swali: Una ushauri gani kwa Serikali ili tuondokane na ugonjwa huu wa wanafunzi kutojua hesabu?
Jibu: Nina imani kwamba, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Rais na wadau wote wa elimu wanatambua kuwa hatuna mtalaa na kuwa tulichonacho ni muhtasari wa mtalaa. Kwa hiyo, mamlaka husika ziandae mtalaa wa masomo unaokidhi mahitaji ya leo na kesho.

Mtaala ambao mtu yeyote anaweza kutumia kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia. Kama mzazi unasafiri na huwezi kumfundisha mwanao, basi uwe na uwezo wa kutumia mtalaa kumwachia kazi mtoto atakayoifanya mpaka urudi.Mtoto mwenyewe  awe na uwezo wa kuutumia.

Suala la  uandishi wa vitabu, liangaliwe upya hasa katika uhariri ambao unapaswa  ufanywe kwa umakini na watu wenye ujuzi wa kutosha katika somo husika.

Kuna machapisho matano ya vitabu vya Hisabati ambavyo vimetolewa bila kuhaririwa.Kwa mfano,
kitabu cha Hisabati darasa la saba, kilichoandikwa na Taasisi ya Elimu Tanzania, kuanzia chapisho lake la kwanza mpaka la tano, kuna  makosa yaliyojirudia katika machapisho haya yote. Hiki hakijahaririwa,  haiwezekani kitabu kiwe na makosa yale yale katika machapisho yote matano.

Swali: Una lolote pia la kuwaeleza wazazi
Jibu: Wazazi wabadilishe mitizamo yao na jinsi wanavyozungumza na watoto wao, waangalie mambo ya kuwaambia watoto. Kumwambia mtoto huwezi chochote na maneno mengine ya kumkatisha tamaa siyo jambo zuri, midomo yetu inaumba.
Swali: Kwa upande wako, upi mchango wako binafsi katika  kukuza hesabu?
Jibu: Kuanzia mwaka 2002, nilikuwa nafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Saalam. Nilifanya kazi pale mpaka mwaka 2005 nilipoacha na kugombea ubunge katika jimbo la Ubungo.

Kwa sasa sifundishi popote, niliona kukaa na kumfundisha mtu mmoja mmoja darasani,  nitakuwa sijatoa mchango wangu kwa jamii yote kama ninavyotaka.Sasa hivi,  naangalia jinsi ambavyo naweza kukaa na kuweza kutoa mchango wangu kwa watu wengi zaidi. Elimu hii iwafikie watu wengi kadri iwezekanavyo, ingawa hata kuzungumza hapa na wewe nawafikia wengi zaidi.

0 comments:

Post a Comment