Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Monday, September 19, 2011

moto mbeya

Jinamizi la majanga ya moto limeendelea kulikumba Jiji la Mbeya baada ya soko lingine la maghorofani lililopo eneo la Forest katika hamashauri hiyo, kuteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha kwa wafanyabiashara.
Tukio hilo limekuja siku mbili tu baada ya soko kubwa la Sido lililopo eneo la Mwanjelwa nalo kuteketea kwa moto Septemba 16, mwaka huu na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha kutokana na maduka na vibanda vya wajasiriamali kuteketea.
Tukio la kuteketea kwa soko la Maghorofani Forest lilitokea usiku wa kuamkia jana saa 9:00 usiku na kuteketeza kabisa maduka manne na vibanda vitano.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema moto huo uligunduliwa na walinzi wa soko hilo ambao walitoa taarifa kwa wenzao wa Chuo cha Uhazini na Grace College kilichopo eneo hilo, ambapo nao walitoa taarifa haraka kwa Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Kufuatia tukio hilo, wakazi wanaoishi karibu na soko hilo walijitokeza na kuanza kuuzima kabla gari la zimamoto halijafika, huku wakiokoa mali zilizokuwemo katika maduka na vibanda hivyo.
Baada ya kuwasili gari la zimamoto, wananchi walishirikiana na askari wa kikosi hicho na hivyo kufanikisha kuuzima baada ya saa moja na hivyo kuepusha madhara kwa vibanda vingine.
Mwenyekiti wa soko hilo, Nadhil Mussa, alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo, alimjulisha Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evance Balama, ambaye alifika muda mfupi kusaidiana na wananchi kuokoa mali za wafanyabiashara hao.
Mussa alisema kutokana na tukio hilo, idadi ya vibanda vilivyoteketea kwa moto ni tisa pamoja na maduka manne, stoo moja ya kuhifadhia mafuta ya kula na meza nne za kupangia bidhaa ndogo ndogo mbalimbali.
Alisema thamani ya mali iliyoteketea bado haijajulikana na kwamba uongozi wa soko utafanya tathmini baadaye kujua hasara kutokana na tukio hilo.
Mwenyekiti huyo alisema katika ajali hiyo hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa na pia vibaka hawakufanikiwa kufika kwenye eneo hilo kwa ajili ya kupora mali kama ilivyotokea ajali ya soko la Sido.
Hata hivyo, Mussa hakueleza chanzo cha ajali hiyo na kwamba uchunguzi wake unafanywa na vyombo vya ulinzi na usalama kwani mfululizo wa matukio ya moto yameanza kuzua hofu kwa wananchi, kwamba huenda kuna jambo ambalo limejificha nyuma yake.
Kutokana na mfululizo wa matukio ya masoko kuungua moto katika Jiji la Mbeya, kumeelezwa na baadhi ya watu kwamba huenda kunatokana na baadhi ya wafanyabiashara kufanyabiashara kwa imani za kishirikina huku wengine wakidai kuwa ni uzembe.

0 comments:

Post a Comment