Subscribe:

Ads 468x60px

.

Tafuta Kila kitu Hapa

Tuesday, September 20, 2011

Ajali yaua abiria wote


Watu sita wamefariki dunia katika ajali mbili tofauti, ikiwemo iliyohusisha watu watano wanaosadikiwa ni ndugu waliokuwa kwenye gari aina ya Toyota Corolla Spacio kufa papo hapo baada ya kugongana uso kwa uso na gari ya mfanyabiashara raia wa Dernmark aina ya Toyota Land Cruiser VX katika eneo la Kirinjiko Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Yusuph Ilembo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa ilitokea Juzi, saa 9:00 alasiri katika barabara kuu ya Moshi-Tanga.
Ilembo alisema Toyota Corola Spasio lenye namba za usajili T 523 BFA lililokuwa likitokea Morogoro kwenda mkoani Arusha likiwa na abiria wanne na kwamba wote walikufa papo hapo na dereva alifia hospitalini.
Alisema gari hilo liligongana uso kwa uso na Toyota Land Cruiser VX yenye namba za usajili T 748 ARA iliyokuwa ikiendeshwa na Ulrik Odd Lind, raia wa Denmark, ambaye pia ni mfanyabiashara na mkazi wa Pangani Mkoa wa Tanga aliyekuwa akitokea mkoani Arusha kwenda Tanga.
Waliokufa katika ajali hiyo ni Godfrey Augustine maarufu kwa jina la Chuwa (26), mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam ambaye ni dereva wa gari aina ya Spacio na abiria wengine wanne waliokuwa ndani ya gari hilo. Wengine ni Julius Abiniel Marika (2); Albert Peter Mbwimbu (58), mfanyabiashara, mkazi wa Tegeta; Christoper Julius (10-12), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Debora iliyoko Babati mkoani Manyara na mwanamume mmoja ambaye hajafahamika jina hadi sasa.
Ilembo alisema dereva wa gari hilo alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Same na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa Spacio uliosababisha kuhama upande wake na kwenda kulia.
Alisema uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea na kwamba dereva wa Land -Cruiser anashikiliwa na polisi katika kituo cha Polisi wilayani Same. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same. Katika tukio lingine, mkazi wa Shirimatunda, mjini Moshi, Edson Seleman (40), amefariki dunia katika ajali iliyotokea eneo la barabara ya Mweka Kibosho wilayani Moshi Vijijini. Watu wengine watatu walijeruhiwa.
Ilembo alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T 160 ANB aina ya Mitsubish Fuso likiendeshwa na Heriel Mzava (35), mkazi wa Soweto.
Alisema gari hilo lilikuwa likitokea Moshi Mjini hilo liliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo na majeruhi.
Waliojeruhiwa ni Jeremia Bazil (28), mkazi wa Shirimatunda; Mohamed Ramadhani (27), mkazi wa Shirimatunda; na Mark Atwai, (21) mkazi wa Kiborlon.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na majeruhi wanaendelea na matibabu hospitalini hapo, ingawa hali zao si nzuri. Dereva wa Fuso alikimbia baada ya ajali.

0 comments:

Post a Comment